Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imejipanga kufanya mabadiliko na mageuzi makubwa katika Taasisi ya Nyaraka na Kumbukumbu kwa lengo la kuongeza ufanisi katika utendaji kazi, hususan katika utunzaji wa nyaraka na kumbukumbu za Taifa.
Ameyasema hayo leo jumapili tarehe 28 Disemba 2025 wakati wa uwekaji wa jiwe la msingi la Afisi ya Taasisi ya Nyaraka na Kumbukumbu Zanzibar, ikiwa ni shamra shamra za maadhimisho ya miaka 62 ya Mapinduzi ya zanzibar.
Amesema jengo hilo litakapokamilika litaweza kukidhi mahitaji ya sasa na ya muda mrefu, kwani limesanifiwa kwa kuzingatia mifumo ya kiusalama, matumizi ya TEHAMA pamoja na mahitaji mbalimbali ya watumishi na wananchi wanaohitaji huduma za nyaraka na kumbukumbu.
Makamu wa Pili wa Rais amesisitiza kuwa ili kufanikisha azma ya kuhifadhi nyaraka na kumbukumbu kwa njia ya kidijitali, ni muhimu kuwajengea uwezo watendaji wa Taasisi hiyo ili kuwa na wataalamu wabobezi wanaokidhi viwango vya kitaifa na kimataifa.
Ameeleza kuwa Serikali itaendelea kutoa ushirikiano na kuunga mkono jitihada zote zitakazohakikisha Zanzibar inajitambulisha kikamilifu katika ramani ya kimataifa kwenye masuala ya nyaraka na kumbukumbu, ikiwa ni pamoja na kuitangaza Zanzibar kihistoria.
Ameongeza kuwa utunzaji bora wa nyaraka na kumbukumbu utachangia katika utafiti mbalimbali na pia kuongeza pato la Taifa kwa kuwa kivutio kwa watalii wanaotembelea Zanzibar.
Makamu wa Pili wa Rais amewataka wafanyakazi wa Taasisi ya Nyaraka na Kumbukumbu kufanya kazi kwa uaminifu na uadilifu mkubwa katika kusimamia hazina hiyo ya Taifa, huku akiahidi kuwa Serikali itaendelea kuwafuatilia kwa karibu ili waweze kufanya kazi kwa weledi na ufanisi.
Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Hemed Abdulla Suleiman akihutubia watendaji wa Taasisi ya Nyaraka na kumbukumbu Zanzibar wakati alipoweka jiwe la Msingi wa jengo jipya la Taasisi ya Nyaraka iliopo kimalani Zanzibar
Meya wa Jiji la Zanzibar, Ndugu Kamal Abdulsatar Haji na viongozi wengine wakisikiliza hotuba ya Mhe Hemed s.Abdullah wakati akihutubia katika ghafla ya uwekaji wa jiwe la msingi.
Watendaji wa Taasisi ya Nyaraka na Kumbukumbu Zanzibar pamoja na wananchi wakisikiliza hotuba ya Mhe Hemed s.Abdullah wakati akihutubia katika ghafla ya uwekaji wa jiwe la msingi.
Makatibu , Wakurugenzi na wajumbe wa bodi ya Taasisi ya Nyaraka na Kumbukumbu Zanzibar wakisikiliza hotuba ya Mhe Hemed s. Abdullah wakati akihutubia katika ghafla ya uwekaji wa jiwe la msingi.