Taasisi ya Nyaraka na Kumbukumbu Zanzibar imeadhimisha Siku ya Nyaraka Duniani kwa
Maonesho yaliolenga kuonesha mchango wa nyaraka katika kuhifadhi na kurithisha maarifa, tamaduni na urithi wa Zanzibar kutoka kizazi kimoja hadi kingine.
Katika maadhimisho hayo, Mgeni rasmi na viongozi mbalimbali walipata fursa ya kutembelea mabanda ya maonesho yaliyohusisha Maulid ya Homu, vikundi vya Dhikri, madrasa za watoto, tiba za asili pamoja na vyakula vya asili vinavyoakisi utamaduni na historia ya Zanzibar.
Mgeni rasmi katika hafla hiyo alikuwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla, akiwa ameambatana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Ikulu, Dkt. Saada Mkuya Salum, pamoja na viongozi wengine kutoka taasisi mbalimbali za ndani na nje ya nchi wakiwemo Mkurugenzi wa Taasisi ya Nyaraka na Kumbukumbu Zanzibar, Ndugu Khatib S Khatib, muwakilishi kutoka Ubalozi wa Norway ndg Oyvind Gressetvold ,Kjersti Larsen, Anne K. Bang pamoja na mkurugenzi wa makumbusho na historia Chuo Kikuuu cha Oslo, Norway.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mhe. Hemed Suleiman Abdulla alisisitiza umuhimu wa nyaraka katika maendeleo ya jamii na Taifa kwa ujumla. Alieleza kuwa kupitia nyaraka wananchi wanaweza kuthibitisha haki zao na kujifunza kutokana na uzoefu wa vizazi vilivyopita.
“Nyaraka si karatasi zinazohifadhiwa maofisini pekee, bali ni hazina muhimu inayobeba historia, utambulisho na mustakabali wa Taifa,” alisema Mhe. Hemed.
Aidha, hafla hiyo ilijumuisha utoaji wa cheti cha shukrani kwa ndg Mustafa Ikbal Abdallah kwa kutambua mchango wake wa kipekee katika kuendeleza na kuimarisha usimamizi wa nyaraka na kumbukumbu.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdulla, akiongozana na viongozi mbalimbali wa Serikali, akipokea maelezo katika banda la maonesho ya vyakula vya asili wakati wa kutembelea mabanda mbalimbali ya maonesho yaliyokuwa sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Nyaraka Duniani.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdulla, akiongozana na viongozi mbalimbali wa Serikali, akipokea maelezo katika banda la katika banda la tiba asili wakati wa ziara ya kutembelea mabanda mbalimbali ya maonesho yaliyokuwa sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Nyaraka Duniani.
Mkurugenzi wa Taasisi ya Nyaraka akitoa maelezo kuhusu nyaraka za Kiislamu na Kiarabu zilizopo katika chumba cha maonesho (Exhibition Room) wakati wa maadhimisho ya Siku ya Nyaraka Duniani, yaliyoambatana na maonesho ya nyaraka za Kiislamu na Kiarabu.
Washiriki wa igizo wakitoa ujumbe kuhusu nafasi ya nyaraka katika kulinda haki za watu na kuhifadhi historia kwa vizazi vijavyo
Mgeni rasmi akihutubia na kufungua rasmi maonesho yaliyofanyika katika maadhimisho ya Siku ya Nyaraka Duniani.
Mgeni rasmi akiwa katika picha ya pamoja na viongozi mbalimbali pamoja na wafanyakazi wa Taasisi ya Nyaraka na Kumbukumbu Zanzibar wakati wa maadhimisho ya Siku ya Nyaraka Duniani.
Miongoni mwa washiriki akitoa Mchango kwa Taasisi ya Nyaraka na kumbukumbu baada ya kupokea mafunzo juu ya usimamizi wa nyaraka na kumbukumbu yaliofanyika Wilaya ya Kaskazini A , Ofisi ya Elimu Mkwajuni.
Wananchi waliohudhuria maadhimisho ya Siku ya Nyaraka Duniani wakipata fursa ya kutembelea banda la vyakula vya asili na kufurahia ladha ya vyakula vya Kizanzibari.