Katika kuadhimisha Juma la Nyaraka , Taasisi ya Nyaraka na Kumbukumbu Zanzibar imeandaa maonesho madogo ya nyaraka za kisheria ikiwa ni sehemu ya shughuli za kuadhimisha Juma la Nyaraka Duniani 2026.
Akizungumza katika ufunguzi wa maonesho hayo, Mgeni Rasmi, Prof. Mohammed Hafidh, amesema kuwa Taasisi imefanya jambo muhimu kwa kuandaa maonesho hayo yenye lengo la kuitangaza Taasisi kwa jamii na kutoa uelewa kuhusu nyaraka na kumbukumbu muhimu zinazohifadhiwa kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
Aidha, Prof. Mohammed aliwahimiza watumishi wa Taasisi kutumia fursa za masomo na mafunzo mbalimbali ili kujiendeleza kitaaluma na kuendana na mabadiliko ya teknolojia katika usimamizi na uhifadhi wa nyaraka kwa njia za kisasa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Taasisi Ndg Khatib Suleiman Khatib alisema kuwa maonesho hayo yameandaliwa kwa lengo la kutoa elimu kwa jamii kuhusu umuhimu wa kutunza nyaraka muhimu kwa matumizi ya sasa na ya baadaye, sambamba na kuhamasisha utamaduni wa kuhifadhi kumbukumbu kwa usahihi na usalama.
Maonesho hayo yamewapa fursa wageni na wadau mbalimbali kujionea baadhi ya nyaraka za kisheria zenye thamani ya kihistoria.
Mkuu wa Kitengo cha Sheria, Taasisi ya Nyaraka na Kumbukumbu Zanzibar, Ndg Anwar Yunus Yahya, akiwakaribisha wageni na kutoa maelezo mafupi kuhusu madhumuni ya maonesho ya nyaraka za kisheria, yaliyolenga kutoa elimu juu ya umuhimu wa utunzaji na uhifadhi wa nyaraka za kisheria kwa matumizi ya sasa na ya baadaye katika kuimarisha utoaji wa haki katika jamii.
Mkurugenzi wa Taasisi ya Nyaraka na Kumbukumbu Zanzibar, Ndg. Khatib Suleiman Khatib, akitoa maelezo mafupi kuhusu umuhimu wa maonesho ya nyaraka za kisheria kabla ya kumkaribisha Mgeni Rasmi kwa ajili ya kutoa nasaha na kufungua rasmi maonesho hayo.
Mgeni Rasmi, Prof. Mohammed Hafidh, akizungumza na wageni pamoja na washiriki mbalimbali kabla ya kufungua rasmi Maonesho ya Nyaraka za Kisheria yaliyoandaliwa na Taasisi ya Nyaraka na Kumbukumbu Zanzibar.
wanafunzi wa vyuo vya sheria, wakifuatilia kwa makini hotuba ya Mgeni Rasmi, Prof. Mohammed Hafidh, kabla ya kufungua rasmi Maonesho ya Nyaraka za Kisheria yaliyoandaliwa na Taasisi ya Nyaraka na Kumbukumbu Zanzibar.
Mgeni Rasmi, Prof. Mohammed Hafidh, akitembelea chumba cha maonesho ya nyaraka za kisheria na kujionea baadhi ya nyaraka za kipekee zinazohifadhiwa na Taasisi ya Nyaraka na Kumbukumbu Zanzibar, sambamba na kutoa maoni na ushauri kuhusu umuhimu wa kuendelea kuhifadhi urithi huo.
Mgeni Rasmi, Prof. Mohammed Hafidh, akipokea tafsiri ya baadhi ya nyaraka za mikataba zilizoandikwa kwa lugha ya Kiarabu kutoka kwa Afisa Kumbukumbu, Bw. Abdallah S. Said, wakati alipotembelea chumba cha maonesho ya nyaraka za kisheria.
Wanafunzi wa Sheria wakiwa katika chumba cha maonesho ya nyaraka za kisheria, wakipata maelezo kutoka kwa Mkuu wa Kitengo cha Sheria kuhusu aina mbalimbali za nyaraka za kisheria za zamani zilizohifadhiwa, zikiwemo mikataba ya kisheria (treaties).
Mgeni Rasmi Prof. Mohammed Hafidh, Mkurugenzi na watendaji wa Taasisi ya Nyaraka na Kumbukumbu wakiwa katika picha ya pamoja katika maonesho ya nyaraka za kisheria,