MKUTANO NA WAANDISHI WA HABARI KUHUSU MAADHIMISHO YA JUMA LA NYARAKA ZANZIBAR 2026

Ndugu Viongozi,
Ndugu Waandishi wa Habari,
Wageni Waalikwa,
Mabibi na Mabwana.

Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.

Napenda kuwakaribisha nyote katika mkutano huu muhimu wenye lengo la kutangaza rasmi maadhimisho ya Juma la Nyaraka Zanzibar kwa mwaka 2026.

Awali ya yote, Taasisi ya Nyaraka na Kumbukumbu Zanzibar inapenda kutoa shukrani za dhati kwa vyombo vya habari kwa mchango mkubwa mnaoutoa katika kuelimisha jamii, kuhabarisha wananchi na kueneza taarifa mbalimbali muhimu kwa maendeleo ya taifa letu.

Ndugu waandishi wa habari,

Maadhimisho ya Siku ya Nyaraka Duniani kwa mwaka huu, yanaongozwa na kaulimbiu isemayo: (Archives for Justice, Rights, Memory and Future) ikiakisi na “Nyaraka kwa Haki, Haki za Binadamu, Kumbukumbu na Mustakabali.” Kaulimbiu hii inaonesha nafasi muhimu ya nyaraka katika kulinda haki za wananchi, kuhifadhi kumbukumbu za taifa, kuimarisha uwajibikaji na kusaidia vizazi vya sasa na vijavyo kupata taarifa sahihi kwa maendeleo endelevu.

 

Ndugu waandishi wa habari,

Siku ya Nyaraka Duniani huadhimishwa kila mwaka ifikapo tarehe 9 Juni kwa lengo la kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa nyaraka na kumbukumbu katika maendeleo ya jamii, uhifadhi wa historia, pamoja na kuimarisha uwazi, uwajibikaji na utawala bora. Maadhimisho haya yaliidhinishwa rasmi na Baraza la Kimataifa la Nyaraka (International Council on Archives – ICA) mwaka 2007 ikiwa ni kumbukumbu ya kuanzishwa kwa baraza hilo tarehe 9 Juni 1948 chini ya mwavuli wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO).

Nyaraka zina nafasi muhimu katika kuhifadhi historia, kulinda haki za wananchi, kusaidia tafiti za kielimu na kuhakikisha upatikanaji wa taarifa sahihi kwa vizazi vya sasa na vijavyo. Aidha, nyaraka ni nyenzo muhimu katika kuimarisha utambulisho wa taifa na kuhifadhi urithi wa kitamaduni wa jamii. Katika kuadhimisha Siku ya Nyaraka Duniani kwa mwaka 2026, Taasisi ya Nyaraka na Kumbukumbu Zanzibar imeandaa shughuli mbalimbali zitakazofanyika kuanzia tarehe 03 hadi 09 Juni 2026 kama ifuatavyo:

  1. Jukwaa la Nyaraka – 03 Juni 2026

Kutafanyika Jukwaa la Nyaraka litakalobeba mada kuu ya Juma la Nyaraka 2026. Jukwaa hilo litawakutanisha wadau mbalimbali kwa ajili ya majadiliano kuhusu umuhimu wa nyaraka na kumbukumbu katika haki, utamaduni, historia na maendeleo ya jamii.

 

  1. Ziara za Kijamii – 04 Juni 2026

Taasisi itatembelea wastaafu wa Taasisi pamoja na watoto yatima katika kituo cha ZASO Children Home kwa lengo la kuonesha mshikamano wa kijamii, kuthamini mchango wa wazee waliolitumikia taifa, pamoja na kusaidia makundi yenye mahitaji maalumu.

  1. Bonanza la Michezo – 06 na 07 Juni 2026

Kutafanyika bonanza la michezo litakalowashirikisha wadau mbalimbali. Tarehe 06 Juni kutakuwa na michuano ya mpira wa miguu kati ya timu za Nyaraka, PBZ, Tawakkal na IPA, ambapo timu zitakazoshinda zitacheza fainali tarehe 07 Juni 2026. Aidha, kutakuwa na michezo watoto ikiwemo mbio za watoto. Bonanza hilo linalenga kuimarisha ushirikiano, afya na mahusiano mema miongoni mwa wafanyakazi na wadau mbalimbali.Mgeni rasmi katika bonanza hilo ni Naibu Waziri wa Habari ,Sanaa ,Utamaduni na Michezo Mhe: Ali Abdulghulam Hussein.

  1. Maonesho ya Nyaraka za Kisheria – 08 Juni 2026

Kutafanyika maonesho maalumu ya nyaraka za kisheria katika Taasisi ya Nyaraka na Kumbukumbu Zanzibar, Kilimani, kuanzia saa 3:00 asubuhi hadi saa 9:00 alasiri.

Maonesho hayo yanalenga kutoa elimu kwa wananchi na wadau kuhusu umuhimu wa nyaraka katika kuhifadhi haki, kumbukumbu na uwajibikaji wa jamii. Wananchi wote wanakaribishwa kushiriki, na hakutakuwa na kiingilio chochote.

  1. Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Nyaraka Duniani – 09 Juni 2026

Kilele cha maadhimisho kitafanyika katika eneo la Makumbusho ya Amani, mkabala na Hospitali ya Mnazi Mmoja.

Sherehe za Maadhimisho hayo yataambatana na maonesho ya Maandiko ya Kiislamu na Hati za Kiarabu, elimu ya Madrasa, tiba za asili, Dhikri, Maulid ya Home pamoja na vyakula vya asili.

Wananchi, wadau na wageni wote wanakaribishwa kushiriki katika shughuli hizo, na hakutakuwa na kiingilio chochote. Na Mgeni Rasmi katika kilele hicho tunatarajia kuwa ni Makamo wa Pili wa Rais Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla.

Ndugu waandishi wa habari,

Kupitia mkutano huu, tunatoa wito kwa wananchi wote, taasisi za serikali na binafsi, wanafunzi, watafiti pamoja na wadau mbalimbali kushiriki kikamilifu katika maadhimisho haya. Vilevile, tunaviomba vyombo vya habari kuendelea kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa nyaraka na kumbukumbu katika maendeleo ya taifa.

Tunawahimiza waandishi wa habari na watafiti kutumia nyaraka kama chanzo muhimu cha taarifa sahihi katika tafiti, makala, vipindi na taarifa mbalimbali zinazolenga kuelimisha jamii. Aidha, tunatoa rai kwa wananchi kuhifadhi nyaraka zao muhimu kwa usalama ili kusaidia kizazi cha sasa na kijacho kupata kumbukumbu sahihi na zenye manufaa kwa taifa.

Ndugu waandishi wa habari,

Taasisi ya Nyaraka na Kumbukumbu Zanzibar itaendelea kutekeleza wajibu wake wa kuhifadhi, kulinda na kusimamia nyaraka kwa mujibu wa sheria, taratibu na misingi ya kitaalamu.

Mwisho, tunawashukuru tena nyote kwa kuitikia wito wetu na kushiriki katika mkutano huu muhimu. Tunawaalika wananchi wote kushiriki katika shughuli zote za maadhimisho haya.

Ahsanteni sana kwa kunisikiliza.

 

MATUKIO KWA PICHA

Waziri wa Nchi Afisi ya Rais – Ikulu Mhe: Dkt Saada Mkuya Salum Akiongea na waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali vya habari Tanania.

Mwandishi wa Habari  wa Kituo cha ITV Zanzibar Ndg Farouk Karim akiuliza swali kwa Mhe Waziri.