Maendeleo na matukio mbalimbali duniani, yameendelea kuwa kielelezo muhimu kinachoonesha umuhimu wa utunzaji wa nyaraka na kumbukumbu kitaifa na kimataifa kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.

Akizungumza katika mafunzo ya kuwajengea uwezo walimu wakuu wa skuli za msingi na sekondari kuhusu usimamizi bora wa nyaraka na kumbukumbu, Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Taasisi ya Nyaraka na Kumbukumbu Zanzibar, ambaye alikuwa mgeni rasmi, Ndg Shekha Makame Mussa, alisema kuwa mwaka 1948, kufuatia athari za vita vya pili vya dunia, Baraza la Kimataifa la Nyaraka (ICA) lilianzishwa kutokana na hofu ya upotevu wa nyaraka muhimu za mataifa mbalimbali.

Alieleza kuwa mwaka 2008, ilipitishwa azimio la kuanzishwa kwa Siku ya Nyaraka Duniani, inayoadhimishwa kila mwaka tarehe 9 Juni, kwa lengo la kuwakumbusha watunga sera na jamii kwa ujumla kuhusu umuhimu wa nyaraka, pamoja na kuondoa dhana potofu kuwa nyaraka ni makaratasi yasiyo na thamani.

Aidha, aliwataka walimu wakuu kutumia mafunzo hayo ipasavyo, akisisitiza kuwa wao ni wazalishaji wakuu wa nyaraka muhimu, hususan takwimu zinazochangia maendeleo ya sekta ya elimu nchini.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Taasisi ya Nyaraka na Kumbukumbu Zanzibar, Ndg Khatibu Suleiman Khatibu, alisema kuwa jukumu la kusimamia na kuhifadhi kumbukumbu ni muhimu ili kuhakikisha zinawanufaisha wananchi na jamii kwa ujumla.

Aliongeza kuwa juhudi hizo zinapaswa kuanzia ngazi ya wilaya hadi mashuleni, ambapo walimu wakuu wanapaswa kuhakikisha nyaraka zinazalishwa na kutunzwa kwa kuzingatia sheria na taratibu zilizowekwa, kwa kushirikiana na taasisi husika.

Pia alisisitiza umuhimu wa mitaala ya elimu kuzingatia zaidi utunzaji wa kumbukumbu, hasa kutokana na changamoto za upotevu na utunzaji usioridhisha wa vyeti na nyaraka za wanafunzi. Alibainisha kuwa hali hiyo imekuwa ikisababisha matatizo kwa wahitimu wanapotafuta ajira kutokana na kukosekana kwa kumbukumbu sahihi baada ya muda mrefu.

Washiriki wa mafunzo hayo, akiwemo Mwalimu Mkuu wa Skuli ya Potoa Msingi, waliishukuru Taasisi ya Nyaraka na Kumbukumbu kwa kuandaa mafunzo hayo, wakieleza kuwa hapo awali hali ya utunzaji wa nyaraka ilikuwa duni, lakini mafunzo hayo yatawasaidia kuboresha utunzaji huo.

Aidha, waliomba elimu hiyo itolewe pia kwa walimu wanaohusika moja kwa moja na masuala ya kumbukumbu, wakiwemo wasajili wa wanafunzi na watumishi wa masjala, ili kuongeza ufanisi katika utunzaji wa nyaraka na kuahidi kuwa mabalozi wazuri wa kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa utunzaji wa kumbukumbu.

 

MATUKIO KWA PICHA

Mkurugenzi wa Taasisi ya Nyaraka na Kumbukumbu Zanzibar Ndg Khatib S. Khatibu akitoa maelezo machache na kumkaribisha mgeni rasmi kufungua mafunzo ya kuwajengea uwezo walimu wakuu wa skuli za sekondari na msingi  juu ya usimamizi wa nyaraka na kumbukumbu yaliofanyika Wilaya ya Kaskazini A , Ofisi ya Elimu  Mkwajuni.

Mwenyekiti wa Bodi ya Ushari Taasisi ya Nyaraka na Kumbukumbu Zanzibar Ndg Sheha Makame Mussa akizungumza na walimu wakuu wa Skuli za msingi na Sekondari katika mafunzo ya kuwajengea uwezo juu ya usimamizi wa nyaraka na kumbukumbu yaliofanyika wilaya ya Kaskazini A Ofisi ya Elimu  Mkwajuni.

Msaidizi Afisa Kumbukumbu ndg Omar Karume Juma akiwasilisha mada ya usimamizi wa nyaraka na kumbukumbu kwa walimu wakuu wa Skuli ya Msingi na Sekondari katika katika mafunzo ya kuwajengea uwezo juu ya usimamizi wa nyaraka na kumbukumbu yaliofanyika Wilaya ya Kaskazini A , Ofisi ya Elimu  Mkwajuni.

 Walimu wakuu wa Skuli za Msingi na Sekondari walioshiriki katika mafunzo ya usimamizi wa Nyaraka na Kumbukumbu Wakisikiliza kwa umakini mafunzo yalioandaliwa na Taasisi ya Nyaraka na Kumbukumbu Zanzibar – Wilaya ya Kaskazini A , Ofisi ya Elimu  Mkwajuni.

Walimu wakuu wa Skuli za Msingi na Sekondari walioshiriki katika mafunzo ya usimamizi wa Nyaraka na Kumbukumbu yalioandaliwa na Taasisi ya Nyaraka na Kumbukukumbu Zanzibar – Wilaya ya Kaskazini A , Ofisi ya Elimu  Mkwajuni.

Mwalimu mkuu wa skuli ya Potoa msingi Ndg Mtumwa M Abdalla akichangia mada katika mafunzo ya usimamizi wa nyaraka na kumbukumbu yaliofanyika Wilaya ya Kaskazini A , Ofisi ya Elimu  Mkwajuni.

Miongoni mwa washiriki  akitoa Mchango kwa Taasisi ya Nyaraka na kumbukumbu baada ya kupokea  mafunzo juu ya  usimamizi wa nyaraka na kumbukumbu yaliofanyika Wilaya ya Kaskazini A , Ofisi ya Elimu  Mkwajuni.

Afisa Elimu Kaskazini A Juma Mwadini Abdallah akijibu maswali ya washiriki wa mafunzo ya usimamizi wa nyaraka na kumbukumbu Wilaya ya Kaskazini A , Ofisi ya Elimu  Mkwajuni.