Mashindano ya Nyaraka Day Cup 2026 yaliyoandaliwa na Taasisi ya Nyaraka na Kumbukumbu Zanzibar kama sehemu ya shamrashamra za kuadhimisha Siku ya Nyaraka Duniani, yamehitimishwa kwa mafanikio baada ya timu ya PBZ Bank kuibuka bingwa wa mashindano hayo.
Mashindano hayo yalizinduliwa rasmi katika Viwanja vya Maisara na Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Taasisi ya Nyaraka na Kumbukumbu Zanzibar, Ndugu Sheha Makame Mussa, ambaye alikuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa michuano hiyo.
Katika hatua ya nusu fainali, timu ya Tawakal Hospital iliibuka na ushindi wa mabao 3–1 dhidi ya IPA, huku PBZ Bank ikiifunga Nyaraka kwa mabao 2–0 na kufanikiwa kutinga fainali.
Mchezo wa fainali uliofanyika katika Viwanja vya Mao Zedong ulikuwa wa ushindani mkubwa ambapo PBZ Bank iliibuka bingwa baada ya kuifunga Tawakal Hospital kwa mabao 3–1 na kutwaa kombe la Nyaraka Day Cup 2026.
Washindi walikabidhiwa kombe pamoja na fedha taslimu, huku mshindi wa pili, wa tatu na wa nne wakipatiwa zawadi mbalimbali. Aidha, washiriki wote wa mashindano hayo walikabidhiwa zawadi za ushiriki kwa kutambua mchango wao katika kufanikisha bonanza hilo.
Sambamba na mashindano hayo, kulifanyika mbio za watoto zilizowashirikisha watoto wa rika mbalimbali, ambapo washindi walipatiwa zawadi tofauti ikiwa ni sehemu ya kuhamasisha ushiriki wa watoto katika shughuli za kijamii na michezo.
Mgeni rasmi katika hafla ya kufunga mashindano hayo alikuwa Mhe. Ali Abdulghulam Hussen, Naibu Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, ambaye aliwapongeza washiriki wote kwa kuonesha ushindani wa kirafiki na kuhimiza kuendelea kutumia michezo kama nyenzo ya kujenga afya, umoja na mshikamano wa jamii.
Mashindano hayo ni miongoni mwa shughuli zilizofanyika katika Juma la Nyaraka 2026, kuelekea kilele cha maadhimisho ya Siku ya Nyaraka Duniani, inayoadhimishwa kila mwaka tarehe 9 Juni.
Wachezaji wa timu za IPA na Tawakal Hospital wakiwa katika picha ya pamoja kabla ya kuanza kwa mchezo wa nusu fainali wa Nyaraka Day Cup 2026, uliofanyika katika Viwanja vya Maisara ikiwa ni sehemu ya shamrashamra za maadhimisho ya Siku ya Nyaraka Duniani
Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Taasisi ya Nyaraka na Kumbukumbu Zanzibar, Ndg. Sheha Makame Mussa, akisalimiana na wachezaji wa timu ya PBZ Bank wakati wa ukaguzi wa timu kabla ya kuanza kwa mchezo dhidi ya timu ya Nyaraka katika mashindano ya Nyaraka Day Cup 2026.
Sehemu ya pambano kali kati ya Tawakal Hospital na IPA katika hatua ya nusu fainali ya mashindano ya Nyaraka Day Cup 2026.
Waamuzi wa mchezo wa fainali wa Nyaraka Day Cup 2026 pamoja na waamuzi wasaidizi wakipiga picha ya pamoja kabla ya kuanza kwa mchezo wa fainali uliowakutanisha PBZ Bank na Tawakal Hospital katika Viwanja vya Mao Zedong.
Mgeni Rasmi, Mhe. Ali Abdulghulam Hussen, Naibu Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, akisalimiana na wachezaji wa timu za PBZ Bank na Tawakal Hospital kabla ya kuanza kwa mchezo wa fainali wa Nyaraka Day Cup 2026 uliofanyika katika Viwanja vya Mao Zedong.
Wachezaji wa PBZ Bank na Tawakal Hospital wakisalimiana kabla ya kuanza kwa mchezo wa fainali wa Nyaraka Day Cup 2026, wakionesha spirit ya michezo na ushindani wa kirafiki katika kusaka ubingwa wa mashindano hayo.
Mgeni Rasmi, Mhe. Ali Abdulghulam Hussen, Naibu Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, akikabidhi kombe la ushindi kwa nahodha wa timu ya PBZ Bank baada ya kutwaa ubingwa wa Nyaraka Day Cup 2026.