Taasisi ya Nyaraka na Kumbukumbu Zanzibar imepokea ugeni wa wanafunzi wa Cohort ya sita mwaka wa masomo 2026/2027 kutoka Skuli ya Sheria Zanzibar (The Law School of Zanzibar),katika ziara ya kimasomo iliyolenga kuwajengea uelewa wa kina kuhusu utunzaji na usimamizi wa nyaraka, hususan nyaraka za kisheria, pamoja na huduma zinazotolewa na Taasisi hiyo.
Wanafunzi hao walitembelea Taasisi hiyo wakiwa chini ya uongozi wa mkufunzi wao, Advocate Rahilat Paul Bakilana, pamoja na Mratibu wa Kozi, Bakari Haji Kirosa, kwa lengo la kujifunza kwa vitendo mifumo na taratibu za uhifadhi na usimamizi wa kumbukumbu.
Kupitia ziara hiyo, wanafunzi walipata fursa ya kufahamu kwa karibu umuhimu wa nyaraka katika uendeshaji wa shughuli za kiserikali na kitaasisi, pamoja na mchango wa Taasisi ya Nyaraka na Kumbukumbu Zanzibar katika kuhifadhi, kuhudumia na kurithisha kumbukumbu za taifa kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
Kwa upande wa wanafunzi, Mahmoud Jamal Hamid na Khadija Yussuf Abrahman walieleza kuwa ziara hiyo imeongeza upeo wao wa kitaaluma kwa kuwapa uelewa wa vitendo kuhusu nafasi ya nyaraka katika taaluma ya sheria, hususan katika uhifadhi wa ushahidi, usimamizi wa kumbukumbu za kisheria na uimarishaji wa utawala bora.
Aidha, Taasisi ya Nyaraka na Kumbukumbu Zanzibar imeeleza kuwa itaendelea kuimarisha ushirikiano na taasisi za elimu kwa lengo la kukuza maarifa, utafiti na uelewa wa kina kuhusu umuhimu wa nyaraka na kumbukumbu katika maendeleo ya Taifa.
Mkuu wa kituo cha Kumbukumbu tuli ndugu Fuad A. Moh’d akiwapa maelezo wanafunzi wa sheria juu ya utunzaji na uhifadhi wa Nyaraka.
Afisa Matibabu Nyaraka akiwapa maelezo wanafunzi wa sheria namna ya kutibu nyaraka (paper restoration) iliochakaa na kupoteza haiba yake.
Mkuu wa Divisheni ya Ushauri na Utafiti, Bi. Tabia M. Khamis, akitoa maelezo kwa wanafunzi wa Skuli ya Sheria kuhusu huduma zinazotolewa katika Divisheni ya Ushauri na Utafiti ya Taasisi ya Nyaraka na Kumbukumbu Zanzibar.
Mkurugenzi , Taasisi ya Nyaraka na Kumbukumbu Zanzibar akiwa katika picha ya pamoja na Wanafunzi wa Cohort ya sita ya mwaka wa masomo 2026/2027 wa skuli ya sheria Zanzibar.