Waziri Ofisi ya Rais – Ikulu, Dk. Saada Mkuya Salum akiambatana na Katibu Mkuu Ofisi ya Rais – Ikulu, Ndugu Saleh Juma Musa amefanya ziara katika Taasisi ya Nyaraka na Kumbukumbu Zanzibar.
Katika ziara hiyo, Waziri alitembelea mradi wa ujenzi wa jengo jipya la Taasisi unaotekelezwa na Kampuni ya Zeccon, Mkandarasi Ali Mbarouk aliwasilisha taarifa ya maendeleo ya ujenzi. ambapo Waziri alisisitiza umuhimu wa kukamilisha na kukabidhi jengo hilo ifikapo mwishoni mwa mwezi Desemba, kama ilivyo kwenye makubaliano. Aidha, alihimiza kuzingatia ubora wa kazi, kasi na ufanisi ili kufikia malengo yaliyopangwa.
Nae Mkurugenzi wa Taasisi Ndugu Khatib Suleiman khatib aliwasilisha taarifa fupi kuhusu historia ya taasisi, majukumu na huduma zinazotolewa, pamoja na umuhimu wa taasisi hiyo katika kuhifadhi na kusimamia nyaraka za Serikali.
Aidha Waziri aliwahimiza wafanyakazi kuendeleza ushirikiano, uwajibikaji na nidhamu katika utendaji wao, akibainisha kuwa misingi hiyo ndiyo siri ya mafanikio ya taasisi yoyote. Katibu Mkuu naye aliwataka watumishi kumpa Waziri ushirikiano mzuri ili kuiwezesha taasisi kuimarisha utendaji wake.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri alisisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano kati ya Taasisi ya Nyaraka na Kumbukumbu Zanzibar na Idara ya Nyaraka na Kumbukumbu Tanzania Bara, akipendekeza kuwepo kwa makubaliano rasmi ya ushirikiano (MoU) yatakayowezesha kubadilishana uzoefu, mafunzo na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma za uhifadhi wa nyaraka.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Raisi Ikulu Mhe Dkt Saada Mkuya Salum akitoa maelekezo ya kina juu ya mradi wa ujenzi wa jengo jipya la Taasisi ya Nyaraka kwa Mkandarasi
Waziri wa Nchi Ofisi ya Raisi Ikulu Mhe Dkt Saada Mkuya Salum akiongea na watendaji wa Taasisi ya Nyaraka na kumbukumbu Zanzibar
Watendaji wa Taasisi ya Nyaraka wakisikiliza maelekezo kutoka kwa mhe Waziri Dkt Saada Mkuya Salum
Picha ya pamoja Waziri wa Nchi Ofisi ya Raisi Ikulu Mhe Dkt Saada Mkuya Salum ,Wakurugenzi na Wajumbe wa Bodi ya ushauri Taasisi ya Nyaraka na Kumbukumbu Zanzibar.